Walioambukizwa Virusi vya corona Kenya wafikia 320

Wagonjwa wengine 17 wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona Kenya na kuongeza idadi ya watu wanaougua ugonjwa huo kufikia 320.

Wizara ya Afya ilitangaza maambukizi hayo ikiongezea kwamba wagonjwa wote walikuwa raia wa Kenya.

Katibu wa kudumu katika wizara hiyo Dkt. Mercy Mwangangi, alisema kwamba kaunti ya Mombasa ina wagonjwa 12 wapya kati ya waliotangazwa huku kaunti ya Nairobi ikifuatia kwa wagonjwa watano.

Dkt Mwangangi amesema kwambwa wagonjwa 15 kati yao walipatikana kupitia uchunguzi wa serikali huku wawili wakiwa katika vituo vya karantini.

Amesema kwamba ni miongoni mwa wagonjwa 668 waliofanyiwa vipimo katika saa 24 zilizopita na kwamba kufikia sasa kaunti ya Nairobi inaogoza kwa waliopimwa ikiwa na takriban watu 478.

Wizara hiyo pia imeripoti idadi ya waliopona nchini Kenya kuwa watu 89 baada ya wagonjwa sita zaidi kuwachiliwa baada ya kuripotiwa kupona virusi hivyo.

”Tunashukuru kwamba Wakenya wanachukulia mwongozo wa kuosha mikono na umakini mkubwa”, alisema bi Mwangangi.

Aliwapongeza wavumbuzi wa nchini kwa kuvumbua vifaa vya kukabiliana na janga la corona.

Hatahivyo amesema kwamba kuna tatizo la Wakenya kutegemea sana vitakasa mikono badala ya kutumia maji na sabuni.

Alitoa wito kwa wanaotoa huduma muhimu kwa Wakenya kufuata maagizo yaliowekwa na serikali kwasababu wako hatarini zaidi kuambukizwa ugonjwa huo.

Vilevile amewataka Wakenya kutochukulia vituo vya karantini kama jela.

Amesema washikadau tofauti wamekuwa wakijadiliana na serikali ili kutafuta njia ya kuwasaidia wale wasioweza kulipa gharama zinazohitajika ili kuwaruhusu kuondoka katika vituo hivyo.

Mkurugenzi wa Afya ya Umma Patrick Amoth, amesema kuwa wizara yake inajaribu kuharakisha mchakato wa kuwapima watu waliowasilishwa katika vituo vya karantini baada ya kukiuka amri ya kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri iliotolewa na serikali.

Amesema kwamba baada ya kupimwa wataruhusiwa kwenda nyumbani ili kujitenga.

Amoth pia amesema kwamba setrikali inajaribu kuimarisha mazingira ya vituo vya karantini.

Wakati huohuo kifaa cha kuosha mikono kilichotengennezwa humu nchini kilizinduliwa.

About Celebu 6164 Articles
Number 1 Online Kenya/East Africa Music Distributions and Promotion, All Rights Reserved. On DJ Celebu website we offer you some DJ Mixtapes, Gengetone, RnB, Hip Hop, Reggae, Gospel, Bongo Flava, Taarab, Asili, Mp3 Audio Downloads, Mp4 Videos Downloads.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*