Swahili News

Waziri Kalemani akerwa na kasi ndogo ya matumizi ya umeme Tabora

[ad_1]

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewataka wakazi wa Mkoa wa Tabora kuongeza kasi ya kutumia umeme unaopatikana mkoani humo kwakuwa matumizi yao yapo chini zaidi kulinganisha na umeme unaozalishwa mkoani humo.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati akikagua shughuli za usambazaji wa umeme vijijini katika Kijiji cha Mizanza na kuwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke wilayani Igunga mkoani Tabora, Aprili 27, 2020.

Dkt. Kalemani alisema kuwa mitambo ya kufua umeme iliyopo mkoani humo inauwezo wakuzalisha Megawati 42 za umeme ili itumike mkoa mzima lakini mpaka sasa matumizi ni Megawati 14 tu.

“Kwa nini ninyi wakazi wa Tabora hamtaki kutumia umeme haliyakuwa tayari miundombinu imewafikia na bei ya kuunganisha ni 27,000 tu! mitambo ya hapa Tabora inauwezo wa kufua umeme wa Megawati 42, ninyi matumizi yenu hayafiki hata nusu ya umeme huo,hii si sawa mtaharibu mitambo yetu kwakuwa mingine italazimika kuzimwa na ikizimwa kwa muda mrefu itaharibika na nchi itapata hasara” alisema Dkt. Kalemani.

Aliwataka Viongozi wa Serikali za Vijiji, Mitaa pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kuunganisha umeme katika nyumba zao.

Vilevile aliwataka wananchi hao kuongeza shughuli za uzalishaji mali kama vile viwanda vidogo vinavyotumia umeme ili kuongeza idadi ya matumizi ya umeme ambao mwingi hupotea kwa kukosa watumiaji hali yakuwa bado wakazi wengi hawana huduma hiyo.

Katika ziara yake hiyo, aliwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kulipia shilingi 27,000 ili waunganishiwe umeme.

Akiwa katika Kijiji cha Mizanza, Dkt. Kalemani aliiagiza TANESCO, kuharakisha upelekaji wa nguzo kijijini hapo, ili kuwapa fursa wakazi wa kijiji hicho kuunganishiwa umeme, hivyo amewataka wakazi  hao kulipia gharama za uunganishwaji na kutandaza nyaya katika nyumba zao.

Aliendelea kusisitiza kuwa miradi ya usambazi umeme vijiji hauna fidia, hivyo wananchi watoe ushirikiano kwa wakandarasi na TANESCO pindi wanapopitisha miundombinu katika maeneo yao kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo.

Hata hivyo aliwataka kutumia wakandarasi walioainishwa na TANESCO na wanaotambulika katika serikali za mitaa na vijiji vyao ili kuepuka vishoka na watu wasiowaaminifu.

Sambasamba na hilo, aliwaeleza kuwa wasikubali kulipia miundombinu ya umeme kama nguzo, nyaya, mashineumba (Transfoma) wala mita za LUKU.

[ad_2]

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close